‘Diamond Ndio Simba!’ Cassypool Ashtua Wengi na Kauli ya Kumsifu Hasimu Wake

Muigizaji mashuhuri wa Kenya, Cassypool, amewaacha wengi vinywa wazi baada ya kumsifia mwanamuziki maarufu wa Tanzania, Diamond Platnumz, kwa kumuita “Simba.”

Akizungumza katika Kaunti ya Mombasa wakati wa kumkaribisha mwanamuziki huyo wa Bongo Flava, Cassypool alimpongeza Diamond kwa mafanikio yake katika muziki wa Afrika.

“Na we ndio Simba, East and Central Africa, wengine ni bure,” alisema Cassypool huku akimweleza Diamond.

Hata hivyo, matamshi haya yamezua mshangao miongoni mwa wengi, hasa ikizingatiwa kuwa hivi majuzi Diamond alikuwa na mvutano mkali na msanii wa Kenya, Willy Paul.

Willy Paul alidai kuwa alidhulumiwa na baadhi ya wasimamizi wa Diamond Platnumz, jambo ambalo liliwakera Wakenya kwa kiasi kikubwa.

Uswahiba wa Diamond Platnumz na Cassypool sasa unatazamwa kwa umakini mkubwa. Hii ni kwa sababu Cassypool alikuwa akimkosoa vikali Diamond mwaka 2023.

Katika mahojiano hayo ya awali, Cassypool alimuita Diamond “mwizi” na “pumbavu,” akidai kuwa Diamond alikataa mahojiano yake yasipeperushwe kwenye Wasafi Media inayomilikiwa na Msanii huyo.

“Mimi namwambia asiwahi kanyaga hapa Kenya,” alisema Cassypool wakati huo.

Mabadiliko ya ghafla ya msimamo wa Cassypool yametafsiriwa kwa njia tofauti na mashabiki wa muziki na wachambuzi wa burudani.

Je, ni ishara ya kusuluhisha tofauti au ni mbinu ya kutafuta umaarufu zaidi? Wakati utafichua.

Leave a Reply